Chadema kumshitaki RC mkoa wa Arusha
NA MWANDISHI WETU
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Arusha (Chadema) kinafanya utaratibu wa kumfungulia mashitaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, dhidi ya kauli zake za uchochezi kwa chama hicho na vitisho kwa Mbunge Godbless Lema ambaye kwa sasa anashikiliwa na Polisi.
Akizungumza na vyombo vya habari jana, Katibu wa chama hicho, Amani Golugwa, alisema tayari wameanza kufuata taratibu za kumfikisha kwenye vyombo vya sheria na karibu wanakamilisha kupitia wanasheria wao wa chama.
Golugwa alisema Mulongo amekuwa kikwazo kikubwa kwa kuwa si mara ya kwanza, kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Chadema na kumtuhumu Lema kwa uongo, hali ambayo hadi kwenye mauaji ya chuo cha Uhasibu ilijitokeza.
Alisema kutokana na hali hiyo hawawezi kupuuzia hali hiyo, kwasababu itazidi kuwaumiza na kubambikiwa kesi zisizo za kwao.
“Tunavyoongea mpaka sasa tayari tumeshawasiliana na wenzetu ambao ni wanasheria wa Chadema na tutamfikisha mahakamani huyu mkuu ili iwe fundisho kubwa... kauli zake za uchochezi na za kutupinga sisi zinatuchosha na mimi kama katibu naona amefilisika kisera na hata kimawazo, kwa kuwa kamwe siwezi kumfananisha hata na mtendaji wangu wa chama yoyote,” aliongeza Golugwa.
Akiongelea kesi inayomkabili Mbunge Lema, alisema kuwa mpaka sasa kesi hiyo haina mlalamikaji lakini vitisho alivyotoa mkuu huyo wa mkoa vinasema kuwa Lema kwa sasa hatabanduka na wala hatachomoka.
Alisema kupitia kwa mwanasheria wao wanajipanga kukabiliana na mkuu huyo wa mkoa.
Awali Wakili wa Mbunge Lema, Humprey Mtui, alisema anashangazwa na kitendo cha jeshi la polisi, kumvunjia heshima mbunge Lema.
Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria Lema angepaswa kuitwa na Polisi na kama angekataa angeweza kuchukuliwa sheria kama hiyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment