Sunday, April 28, 2013

Lema kizimbani Arusha leo



Dar/mikoani. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema anafikishwa mahakamani leo kwa madai ya kuchochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu Arusha, huku ikielezwa kwamba jiji hilo litakuwa katika ulinzi mkali.
Ulinzi umeimarishwa maradufu katika mitaa yote jijini Arusha na Kituo Kikuu cha Polisi anakoshikiliwa mbunge huyo tangu usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita.
Lema anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo akidaiwa kuchochea vurugu katika chuo hicho baada ya wanafunzi kuchachamaa kutokana na mauaji ya mwenzao, Henry Kago aliyeuawa kwa kisu karibu na chuo hicho, Jumanne iliyopita.
Ingawa Jeshi la Polisi linadai ulinzi huo ni jukumu lao la kawaida la kila siku, lakini wingi wa askari mitaani umechagizwa na tukio la kukamatwa na kufikishwa mahakamani leo kwa Lema suala linalotokana na rekodi ya wafuasi wa Chadema hasa kukiwa na jambo linalomhusisha mbunge wao na polisi.
Tangu baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2010, wafuasi, wapenzi na viongozi wa Chadema Arusha na kitaifa wamekabiliana mara kadhaa na Polisi mkoani hapa na moja ya matukio yanayokumbukwa ni lile la maandamano ya Januari 5, 2011 lililoishia kwa mauaji ya watu wawili huku viongozi kadhaa wa chama hicho wakifunguliwa kesi ya kusanyiko lisilo halali.
Viongozi wa Chadema wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa, Lema, wabunge kadhaa na viongozi wa ngazi ya wilaya na mikoa. Polisi kutoka wilaya jirani na Arusha za Arumeru, Monduli, Karatu na Longido wanahusika katika ulinzi huo ulioimarishwa tangu juzi.
Wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani wamekuwa na desturi ya kujaa mahakamani pale viongozi wao wanaposhtakiwa kwa kosa lolote na hutoka kwa maandamano yasiyo rasmi kila kesi inapoahirishwa, jambo ambalo limekuwa likizua mvutano kati yao na polisi na aghalabu kuishia kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na baadhi kutiwa mbaroni.
Ulinzi mkali ‘selo’ ya Lema
Polisi wameimarisha ulinzi katika eneo lote la Kituo Kikuu anakoshikiliwa mbunge huyo tangu Ijumaa iliyopita na tangu siku hiyo, watu ambao wamekuwa wakifika hapo kwa sababu mbalimbali wamelazimika kujieleza kwanza kwa askari wa doria kabla ya kuruhusiwa kukaribia lango la kituo hicho.
Katika mitaa mbalimbali nako kuna askari wenye silaha wanaotembea kwa miguu wakiwa wawiliwawili hadi watatu pamoja wale wa pikipiki na wa kikosi cha mbwa na farasi.
Kesi nyingine kubwa za leo
Mbali na kesi hiyo, huenda leo Mahakama Kuu ikatoa uamuzi wa maombi ya Jamhuri katika rufani ya kesi ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Jerry Murro na wenzake wawili.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam inatarajiwa kutoa uamuzi wa kama Muro na wenzake wawili, Edmund Kapama maarufu kama ‘Dokta’ na Deogratius Mugassa wapandishwe kizimbani tena na kuanza kusikiliza upya kesi ya rushwa iliyokuwa ikiwakabili au la.
Kesi nyingine ni ya anayedaiwa kumuua Padre Evaristus Mushi ambaye atapandishwa kizimbani kwa mara ya tatu.


Mtuhumiwa huyo, Omar Yusufu Makame, mkazi wa Mwanakwerekwe, Unguja alikamatwa Machi 29, mwaka huu baada ya uchunguzi uliofanywa na wapelelezi wa Tanzania walioshirikiana na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI). Pia leo kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) Ltd, Iddi Simba na wenzake na inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
                                      source;MWANANCHI JUMATATU.

No comments:

Post a Comment