Tuesday, April 30, 2013

"KUNA MAJAMBAZI WAMETUMWA NA VIGOGO WAJE KUNIUA".......MAMA ZITTO...!!

SHIDA Salum ambaye ni mama mzazi wa mwanasiasa machachari ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amesema kuna watu wanataka kumuua. 



Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu Jumamosi iliyopita, Shida alisema Aprili 19, mwaka huu, saa moja na nusu katika Ghorofa la NSSF maeneo ya Tabata Bima, hawezi kuisahau kwa kuwa ndiyo siku ambayo majambazi walimvamia wakiwa na bastola.
Akisimulia mkasa huo Shida alikuwa na haya ya kusema:
“Majambazi hayo yaliyonivamia siyajui lakini mmoja wao huwa namuona. Kabla hawajaja walinipigia simu wakaniambia wana shida na mimi lakini hatukupanga namna ya kuonana.
Uwazi: Sasa walipofika nyumbani kwako, uliwakaribishaje?
Shida: Walipofika walivamia na kufanikiwa kuingia sebuleni.
Uwazi: Baada ya kuingia ikawaje?
Shida: Cha kwanza walichotaka ni laptop (Kompyuta mpakato), flash na simu zangu.
Uwazi: Uliwapa?
Shida: Baada ya kutoa amri hiyo niliwajibu kuwa kompyuta iko ofisini na simu niliwaambia ziko kwenye chaji.
Uwazi: Baada ya hapo ikawaje?
Shida: Mmoja wa majambazi hayo alinionyesha bastola kuwa kama sijatii hayo wanayoniambia basi watanifanya kitu kibaya,   ndipo nikamuita kijana wangu aitwaye Mtana aende chumbani kuchukua simu zangu niwape.
Uwazi: Ikawaje?
Shida: Niligundua kuwa Mtana alikuwa anasikia amri zilizokuwa zikitolewa na majambazi hayo, hivyo alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi.
Uwazi: Majambazi wakafanya nini?
Shida: Waliposikia kelele walikimbilia nje, wakaingia ndani ya gari lao ambalo namba zake zisijui, wakatoweka.
Uwazi: Pole sana.
Shida: Pamoja na purukushani hizo namshukuru Mungu sana kwa kuwa hawakunidhuru na hawakufanikiwa kuchukua chochote.
Uwazi lilitinga nyumbani kwa mama huyo na kukuta ulinzi ukiwa umeimarishwa ambapo sasa kuna askari wenye bunduki.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, majambazi hayo yalifanikiwa kuingia ndani baada ya mlinzi aliyekuwepo zamu kwenda kubadili nguo za kiraia ili avae za kiaskari.
“Tukio lilikuwa la haraka sana, wakati askari huyo anatoka kwenye kibanda cha kubadilishia nguo ndipo na wale majambazi walipokuwa wakitoka ndani na kuingia kwenye gari lao,” kilisema chanzo.
Waandishi wetu walimtafuta kiongozi wa walinzi wanaolinda nyumbani kwa mama huyo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Ngosha na alipoulizwa kuhusu sakata la kuvamiwa alikiri kulifahamu.
“Baada ya tukio lile tumeimarisha ulinzi ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao. Sasa tumeweka askari wenye bunduki na tunaamini tukio kama hilo halitajirudia,” alisema Ngosha.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Marietha Minagi alikiri kutokea kwa tukio hilo.
“Nina taarifa ya tukio hilo na tunaendelea na upelelezi kuwasaka majambazi hao, wananchi waondoe hofu.” alisema Kamanda Minagi.

No comments:

Post a Comment