MAPENZI NA MAHUSIANO

KUTOA ASANTE YA MWILI NI KUJIDHALILISHA.

NINA imani wote m’wazima wa afya njema kwa uwezo wake Manani.  Leo nataka nizungumzie tofauti ya upendo na msaada.  Sote tunajua katika penzi la kweli kuna kujaliana katika shida na raha na kuonyesha upendo wa mtu kwa mwenzake.
Tunajua wote katika mapenzi  kuna kupendana ili kukamilisha pea ya upendo ikimaanisha kila mmoja ampende mwenzake kwa dhati.

Penzi la upande mmoja tumeona si kamili kwa vile mpendaji huwa mmoja na mwingine huwa yupo na mwenzake kwa sababu fulani, akishakidhi haja zake huondoka bila kwa heri na kusababisha mateso kwa mmoja.

Kuna tatizo limejitokeza kwa kina dada kuamini mtu anayempa msaada basi anamhitaji kimapenzi. Kweli anayekusaidia lazima atakuwa mtu anayejua utu wa mtu bila kuangalia anakujua au la.
Sehemu hii imekuwa ikiwachanganya wengi na kuingia kichwakichwa mwisho kuachwa njia panda na kuona umegeukwa, yaani mtu uliyemuamini amekugeuka.

Kwa nini?
Upendo na msaada ni vitu viwili tofauti, msaada umo ndani ya upendo kwa maana anayekupenda atakusaidia katika shida na raha, lakini si kila msaada una upendo.


Kwa sababu gani?
Tumeona kwenye usafiri wanawake wamekuwa viumbe dhaifu pale wanapopewa msaada na mwanaume na huamini msaada ule ni dalili za kupendwa, kumbe aliyetoa msaada hakutoa kama sehemu ya kuonyesha anakuhitaji kimapenzi bali kukusaidia kama mwanadamu mwenzake.

Wanawake wengi wamekuwa wakipoteza dira ya maisha kwa kuanzisha uhusiano na mtu anayekutana naye safarini na kumpa msaada kama chakula au kumsaidia mtoto. Baada ya msaada huo mioyo yao huwa dhaifu na kuamini yule ndiye mwanaume sahihi kwa vile kamsaidia bila kumjua pengine msaada huo haupati kwa mwenza wake.
Mara moja huanzisha uhusiano na kupeana namba za simu ili watafutane baadaye. Wanawake wengi hufikia hatua ya kuzikana ndoa zao kwa vile tayari mioyo yao imeishakurupuka bila kufikiri.

Wengi wao wamekuwa wakifunga hata safari kuwafuata watu hao hata kama ni mbali bila kuijua historia ya mtu waliyekutana naye kwenye gari.
Baada ya kukutana ndipo wanapokutana na tabia tofauti na waliyoifikiria, hapo ndipo yanakuja majuto. Wapo wanaodiriki kuvunja hata uhusiano wao kwa penzi la mwanaume wa safarini na kuamini aliyekuwa naye si lolote si chochote kwa mwanaume aliyekutana naye.

Hata kama hakumfuata, hicho huwa chanzo cha nyumba kuvunjika au kuingia kwenye migogoro kwa vile  akili yao wameihamishia kwa mwanaume wasiyemjua.
Baada ya kuachwa anaangukia pua kwa vile yule mtu aliyetoa msaada haukuwa kwa lengo ya kumvuta kimapenzi.

Hivyo, inatakiwa tuwe makini sana na uamuzi wetu wa kukurupuka, si kila msaada unaopewa asante yake ni kumvulia nguo mwanaume. Utawavulia nguo wangapi watakaokusaidia?  Kumbuka kusaidiwa ni haki yako kama mwanadamu na si kwa ajili ya kudhalilishwa.

Uheshimu utu na mwili wako, kwa sababu heshima ya mtu huijenga mwenyewe hujengewi na mtu. Usikubali kuutoa mwili wako kama asante kwa msaada utakaopewa, asante ya domo inatosha.

Kama mtatongozana hiyo ni hiyari yenu kukubali au kukataa,  uwe muwazi ili kujiweka eneo salama kwa kuheshimiwa na si kuukana uhusiano wao kwa vile tu umenunuliwa chipsi na kuku pengine soda na kitafunwa.
Akitoa ni kwa upendo wake una haki ya kukubali au kukataa si kila upewacho lazima ukubali kuchukua na asante yako ni kuutoa asusa mwili wako!
Tukutane wiki ijayo.








***************************************************************************

Fanya haya! Unapotokea kumpenda mtu aliye na mpenzi wake,

Tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuonana tena wiki hii tukiwa wazima. Lakini pia tumshukuru kwa kutuletea kitu kinachoitwa mapenzi. 

Mapenzi yamekuwa yakichukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku na yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa furaha kwa kila mtu. 

Kama huamini, angalia wale waliotokea kupenda na wao wakapendwa, utabaini nyuso zao zimetawaliwa na
furaha isiyo na kifani. Lakini mapenzi hayo hayo yamekuwa ni chanzo cha vilio kwa baadhi ya watu. 

Mpenzi msomaji wangu, kupenda hakuna macho! Moyo ukishapenda hausikii la kuambiwa. Katika hili ndiyo maana unaweza kumuona mwanaume kazimika kwa demu ambaye hawaendani kabisa lakini moyo wake ndiyo umeshapenda. 

Ilishawahi kutokea msichana akampenda kijana mmoja ambaye ni fukara kupita maelezo. Yeye akawa ndiyo anamhudumia kwa kila kitu. Akamfanyia mpango wa ajira na mwisho wake wakafunga ndoa. 

Sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na amani. Wamegeuka mfano wa kuigwa kwa jinsi wanavyopendana lakini huko nyuma msichana huyo alikuwa akichekwa kwa kutoa penzi kwa mwanaume asiye na mbele wala nyuma. 

Hayo ndiyo mapenzi jamani! Lakini pia katika kufurukuta kumtafuta mpenzi wa kuwa naye maishani, mwanaume anaweza kujikuta unaangukia kwa demu ambaye tayari ana mpenzi wake. 

Moyo wako unakuambia yeye ndiye mtu sahihi katika maisha yako lakini tayari ana mtu wake, unafanyaje? 

Utapambana kuhakikisha unapata kile ambacho moyo wako umekipenda au utakubaliana na ukweli kwamba huwezi kuwa naye kwa kuwa ana mtu wake? Inapofikia hatua hiyo unaweza kujikuta upo njia panda hasa pale ambapo huyo mwenye mtu wake naye anaonesha kuwa na chembechembe za mapenzi kwako. 
Kuna mambo kadhaa ya kukusaidia kukabiliana na hali hii. 

Chunguza 
Tumia muda wako mwingi kuchunguza juu ya uhusiano wake. Uhusiano wao umesimama na wanaonekana ni watu wenye ‘future’? Nasema hivyo kwa sababu, yawezekana uhusiano wa huyo uliyetokea kumpenda ni wa kuzuga tu na huenda wewe ndiye mwenye ‘future’ naye. Ndiyo maana nikasema chunguza uhusiano wake kwanza. 

Usitafute uadui 
Baada ya kuchunguza, ukibaini kwamba uhusiano wao hauko ‘siriasi’, vuta subira, lolote linaweza kutokea na likaufurahisha moyo wako. Lakini kama utaona ni watu walio siriasi na wanaelekea kuoana, usitafute uadui bure, kaa pembeni. 

Una nafasi kwake? 
Sawa umetokea kumpenda msichana aliye na mtu wake, umeshawahi kujiuliza kama una nafasi ndani ya moyo wake? Anaonesha dalili fulani za kukupenda kama unavyompenda na ni mtu anayeonesha kukumisi anapokuwa mbali na wewe? Utakapobaini una nafasi kwake, uamuzi wa kumpotezea hautakuwa na nafasi. 

Ni rahisi kubadili uamuzi wake? 
Unadhani huyo uliyetokea kumpenda anaweza kubadili maamuzi ya kumuacha huyo aliyenaye kama kweli hawana ‘future’? Utagundua hilo kwa kuongea naye na kumsikia kama anaweza kufanya maamuzi hayo ili awe na wewe. 

Pingana na moyo wako 
Ifike wakati upingane na moyo wako. Unajua moyo wako kukuambia kuwa unataka kuwa na uhusiano na demu ambaye tayari ana mpenzi wake wakati mwingine utakuwa unakupotosha. 

Kwa hiyo ukiona vipi, pingana nao. Acha kumng’ang’ania msichana mwenye mpenzi wake licha ya ukweli kwamba, huenda wewe ndiye mwenye nafasi ya kuwa mume wake na siyo huyo aliye naye. 

Urafiki ni poa? 
Umempenda sana na hauko tayari kumkosa katika maisha yako lakini imetokea kwamba tayari yuko na mtu na umebaini huna nafasi kwake kabisa? Usiumie, omba angalau urafiki. Siyo urafiki wa kivile sana ila angalau pale unapotaka kusikia sauti yake kwa kumsalimia tu, upate nafasi hiyo. 

Usiumie, yupo mwingine 
Haina haja ya kujitafutia vidonda vya tumbo bure kwa kuwa tu umebaini uliyetokea kumpenda tayari ana mtu. Chukulia ni hali ya kawaida, mademu wazuri ambao wanaishi singo wapo kibao huko mtaani, ni suala la wewe kutulia tu. Amini yupo mwingine ambaye atayafanya maisha yako yawe ya furaha. 

Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba, unapotokea kumpenda mtu fulani, pambana kuhakikisha unampata kwa sababu ukimkosa maisha yako yanaweza kuwa gizani. Ila pale utakapoona uwezekano wa kuwa naye haupo, usilazimishe ndugu yangu. Kumbuka haya ni maisha tu!


**********************************************************************************************




Wajua jinsi ya kumdhibiti mpenzi anayepiga mizinga?

Nazungumzia juu ya tabia za baadhi ya watu walio katika uhusiano kupenda kuwapiga 'mizinga' sana wenzi wao. Tabia hii ipo zaidi kwa upande wa wanawake, ingawa siku hizi hata wanaume nao wameingia katika mkumbo huu.

Siyo ajabu kumsikia mwingine akisema; "Mimi nina kibuzi changu bwana kila ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nitakitosa tu, yaani nakichuna kama sina akili nzuri, maisha yanaendelea. Yaani ni full kujiachia."

Si hivyo tu, wapo wanaume ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama watajishughulisha.

Unaweza kumsikia mwanaume akisema; "Aaah! Yule demu kazimika ile mbaya na mapigo yangu, kila ninachotaka ananinpa anajua akinizingua namtosa, hadi mshahara wake akipata ananigawia. Yule ndiyo mwanamke wa kuwa naye bwana!"

Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na pesa, ukiona mpenzi wako anaweka pesa mbele na ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.

Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze kwamba huna kisha muangalie jinsi gani mnaweza kusaidiana katika kutatua tatizo linalomkabili.

Itakuwa sio busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona kwamba unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana, na hili ni kwa pande zote mbili.

Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akutoe ?out?, bila kujali kwamba wakati huo mpenzi wako ana fedha au hana. Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka?

Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu nani? Fanya mabadiliko tafadhali. Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba pesa kila wakati tena katika matumizi mengine ambayo sio ya msingi, vipengele vifuatavyo vinafaa sana kwako...

MWELEZE UKWELI
Kama huna pesa wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile. Mwanaume hatakiwi afahamike siku ana pesa au hana. Maana kuna wenzangu ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye ataongeza ?mizinga? ili afaidi.

Ishi kawaida, kuwa mkweli kwake siku zote, utakapokuwa mkweli kwake atakuheshimu kwa uwazi wako. Siku zote zilingane, uwe una fedha au huna asijue, hilo litakusaidia kwa kiwango kikubwa sana katika maisha yako ya kimapenzi.

JENGA MAZINGIRA YA YEYE KUKUSAIDIA
Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa! Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya daladala analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake. Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna pesa zinavyokuwa hazitoshi na akaweza kubana matumizi.

BANA MATUMIZI
Kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa pesa kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa wewe unazo! Wakati akiwa anaamini hivyo, ukweli ulionao moyoni ni kwamba huna fedha za kutosha.

Unachotakiwa kufanya mapema ni kudhibiti matumizi yako hata kama pesa zinakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakusababishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri kumbe ni kapuku tu.

Kwa kumalizia niseme tu kwamba, mapenzi si kukomoana, mapenzi ni kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku moja na wewe ukiwa na tatizo akusaidie. Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga 'mizinga' mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.

NAWAPENDA SANA!!!





*********************************************************************************

Sifa 10 za kumtambua Mpenzi wa Kweli









Vijana wengi ambao wanapendana leo mapenzi yao hayadumu kiasi cha kubatizwa jina la utamu wa bazoka. Lakini yote hii inatokana na ukweli kwamba elimu ya mapenzi ambayo ni muhimu kwa binadamu haitolewi ipasavyo.

Ipo zana potofu kwamba kumfundisha mtoto mapenzi ni kumharibu, jambo ambalo si kweli bali inategemea mtoto huyo anafundishwa nini na kwa wakati gani. Lakini cha kushangaza zaidi hata watu wazima ambao ni wadau wa mapenzi hawayajui, matokeo yake wanajiingiza kwenye uhusiano wakiwa bumbumbu na hivyo kuteshwa na changamoto zinazowakabili.
Leo tutajifunza kwa undani sifa kumi za mpenzi bora ili tuweze kuwatambua wapenzi wetu kabla ya kuwapa mioyo na utu wetu. Sifa hizo ni hizi zifuatazo.

1.Mpenzi wa kweli ni yule ambaye hatangoja kujua nini unahitaji yaani hana sababu ya kusubiri kuombwa ndiyo atoe msaada.

2. Ni yule atakayejua wakati gani huna furaha au una furaha na atakuwa na wewe kwa hali zote mbili .

3. Ni yule atayekuwa tayari kukusikiliza kwa kile utakachosema, hatojali umeongea baya au zuri

4.Atakuwa na wewe wakati wa shida na raha. Hatakuwa mtu wa kuvizia vizia na kujisogeza wakati ukiwa na raha.

5. Mpenzi wa kweli atakuheshimu na hatopenda kuwa kikwazo cha maisha yako, atakulinda daima.

6. Atakupenda kwa moyo wake wote na wala si kwa ajili ya shinikizo fulani (pesa au mali)

7. Mpenzi wa kweli ni yule atakayeonyesha kuthamini nafasi yako kama rafiki au mpenzi mbele ya wengine, hafichi hisia zake mbele za watu, atakutetea na kukufanya wa kwanza.

8. Kwenye ukweli mpenzi mzuri atasema bila kukuficha na atapenda kukuonyesha mifano ya namna ya kuwa mkweli na mwaminifu.

9.Mpenzi wa kweli ni yule anayejiamini, asiyeyumba katika maamuzi hata kama atalazimika kufanya maamuzi magumu .

10.Atakuwa tayari kuvumilia, hatakuwa mwepesi wa hasira wala kutumia lugha chafu na ubabe.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kuna aina nyingi sana za mapenzi miongoni mwa binadamu. Hivyo ni muhimu kufahamu kuwa kupenda kwa mtu mmoja au watu kadhaa hakuwezi kulinganishwa na wengine kwa mazingira na mienendo.

Wakati fulani niliwahi kufanya uchunguzi miongoni mwa wapenzi ambapo nilikuwa nawauliza swali. “Vipi dada/ kaka, huyu ni mpenzi wako?” Wengi kati ya niliowauliza hawakupoteza hata nusu sekunde kujibu ‘NDIYO’.

Lakini watu hao hao nilipowauliza kwa mara nyingine “Unampenda kwa sababu gani?” Majibu ya wengi yalikuwa na sababu ambazo si za msingi na wengine walinyamaza au kuambulia kucheka.

Hebu wakati tunaendelea na mada hii, jiulize wewe mwenyewe ambaye una mke/mume swali kama hilo unampendea nini huyo mpenzi wako? Baada ya hapo sababu zinaweza kuwa ni kama zifuatazo “ Nampenda kwa sababu ni mzuri wa sura, tabia, umbo, na kusema kweli ananivutia” la kama hizo hazitakuwa sababu sina shaka nawe utanyamaza au utacheka.

Hii ina maana kuwa watu wengi ambao tuna wapenzi iwe wake au waume zetu, huenda tuliwapenda au tunawapenda hadi sasa bila kufahamu kwa nini tunawapenda na kitu gani kilitufanya tuwe wapenzi. Maana ikiwa ni uzuri, tabia, mvuto na sababu nyinginezo, basi lazima tufahamu kuwa uhai wa mapenzi yetu ni mdogo.

Inasemwa hivyo kwa sababu watu hubadilika tabia, sura, umbo, mvuto, ufahamu na hivyo kuweka ukomo wa mapenzi kuwa ni baada ya kutokea kwa mabadiliko hayo ambayo ni ya kawaida katika maisha ya mwanadamu, kwani ni wazi kwamba hakuna kinachodumu miongoni mwa hivyo vinavyotajwa na wengi kama sababu za kupendana.

Watalaam wa elimu nafsi na hasa Bw. Robert Stenberg walijitahidi sana kufanyia utafiti wa mapenzi na kuibuka na aina kuu kiasi cha nne ambazo wanazitaja kuwa ni PENZI LA UTIIFU, PENZI LA KUJALIANA, PENZI LA UIGIZAJI NA PENZI TIMILIFU.


Ufafanuzi unaotolewa na wataalamu hawa unaonyesha dhahiri makosa yanayoweza kufanywa na binadamu katika kuchagua au kupata wapenzi. Jambo ambalo limepelekea kuporomoka kwa uhusiano mwingi kati ya wanaume na wanawake. Wanasema penzi kamili linatakiwa kuwa na sifa tatu, ambazo ni tendo la ndoa, ukaribu na kujitolea.

PENZI LA UTIIFU

Penzi la utiifu au kama wengi wanavyolifahamu hujulikana kama ‘penzi la mahaba’. Katika aina hii ya penzi, wanaopendana hujali sana na kuendekeza zaidi miito ya kimwili. Mapenzi ya kiwango cha juu kabisa miongoni mwao hupatikana pale wanaposhiriki tendo la ndoa. Pia wanaopendana hupenda kuwa pamoja au karibu kwa muda mwingi.

Lakini kwa bahati mbaya penzi la aina hii linakosa sifa moja ambayo ni kujitolea. Wapenzi kwenye penzi hili huonekana na pengine hujiona kuwa wanapendana, lakini unapofika wakati ambapo kujitolea kunahitajika, penzi lililoonekana kushamiri hupukutika ghafla.

Kujitolea kunaweza kuwa na maana ya kuumia kwa ajili ya mwingine, kutoyumbishwa na watu wa pembeni na kuwa tayari kulinda penzi hilo kwa gharama yoyote. Kwa mfano ukiona mpenzi wako hayuko tayari kukusaidia unapoumwa, unapokuwa na matatizo, hakuhurumii unapokuwa taabuni ujue kuwa mapenzi yenu ni ya utiifu ambayo uhai wake ni mdogo.

Jambo la kufanya hapa ni kwa wapenzi wenyewe kujitambua na kuchukua hatua za kukamilisha pengo la kujaliana ili kutowapa nafasi wambea na shida za dunia kuyumbisha meli ya penzi ambayo wanasafiria, ikishindikana watu hawa wanashauriwa kutokuwa wepesi wa kuoana kwani uwezekano wa ndoa yao kutodumu ni mkubwa.

PENZI LA KUJALIANA

Penzi la kujaliana ni lile ambalo wanaopendana wanakuwa karibu mara zote na kushiriki mambo mengi pamoja. Wapenzi wa kundi hili huwa na hali ya kujitolea tofauti na penzi la utiifu ambalo tumeliangalia, lakini kasoro yao kubwa huwa kwenye miito ya mwili. Jambo la kufurahisha hapa ni kwamba wapenzi wa kundi hili wako makini kwa kila sehemu na mara nyingi huwa hawakubali kuingiliwa maamuzi ya mapenzi yao.

Lakini linapokuja suala la tando la ndoa hujitokeza kasoro nyingi za kutofikishana kileleni au kutofurahishana na hivyo anguko lao huletwa na muwasho wa mwili ambao huwasukuma wapendanao hao kutoka ndani ya uhusiano wao na kufanya usaliti.

Sasa ili kulifanya penzi la aina hii liwe imara lazima wapenzi waulizane kuhusu kutimiziana haja za mwili wanapokuwa faragha. Kama kuna kasoro kati yao si busara kufichana wanatakiwa kuwaona wataalamu wa mapenzi na kupata ushauri utakaosaidia kuondoa tatizo hilo. Hawa pia wanashauriwa kutooana haraka.

PENZI LA UIGIZAJI

Penzi la aina ya tatu linalotajwa na watafiti ni lile lijulikanalo kama penzi la Uigizaji. Hili ni lile penzi ambalo wanaopendana hukutana asubuhi na ikifika jioni tayari ni wapenzi kamili, ambapo hugandamana kama ruba, utadhani waigizaji wako kwenye matayarisho ya filamu. Ukiwatazama wanakuwa kama vichaa na msukumo wao wa kutimiza hisia za mwili huwa ni mkubwa kiasi cha kufikia kufanya mapenzi hata barabarani au kwenye sehemu za wazi.

Wapenzi wa aina hii huchukua muda mfupi sana kutangaziana mambo ya ndoa na pengine kuoana bila kufahamiana zaidi kitabia. Wanajuana asubuhi na jioni mwanamke/mwanaume keshahamia kwa mwenzake na maisha yanaanza, hapo hakuna ushauri wala muongozo wa watu wengine.

Tatizo kubwa ambalo hujitokeza katika penzi la aina hii ni wapenzi kuchokana mapema na hamu ya kufanya tendo la ndoa kupotea. “Yaani nikiwa na mume wangu sijisikii kabisa kufanya naye mapenzi, lakini kwa wengine nakuwa na hamu sana” hizi ni kauli za wapenzi wa penzi la kisinema sinema.

Mbali na hilo wapenzi wa aina hii ni rahisi kuporwa na kuanzisha uhusiano mpya, hivyo inashauriwa kuwa kwa wale ambao wanaona kuwa wako kwenye kundi hili, wajitahidi kujizuia na kupeana nafasi za kujuana zaidi kupitia ushauri wa watu wengine. Si vema kushiriki tendo la ndoa kila mara kwa staili na sehemu zile zile na pia haifai kukurupuka kuoana bila kuchunguzana tabia, ndoa za hivi hazidumu.


PENZI TIMILIFU

Aina ya mwisho ya penzi kama inavyoelezwa na mtaalamu Sternberq ni ile ya penzi timilifu. Aina hii ya mapenzi inakuwa na sifa zote tatu, yaani TENDO LA NDOA. Kwamba wapendanao huwa hawana kasoro katika eneo hili, unapofika muda wa kupeana raha hufikishana mahali pa juu. UKARIBU kwamba muda wote huwa karibu na kila mmoja hakai na kiu ya kutokumuona mwenzake kiasi cha kupoteza hisia na kushawishika kufanya usaliti.

Sifa ya mwisho ni KUJITOLEA. Ni mahodari kusaidiana, kufarijiana na hawako tayari kupokea mambo kutoka pembeni yanayohusu uhusiano wao, hivyo huwa si rahisi kwao kuyumba kwa sababu za umbea. Kumbuka katika penzi hili tendo la ndoa huwa si sehemu muhimu sana kwa wapenzi, yaani kwao penzi ni rohoni zaidi kuliko mwilini hata wakikaa muda wa miezi mitano bila kufanya tendo la ndoa upendo wao haupungui.

Hata hivyo, penzi la aina hii kwa mujibu wa wataalamu ni vigumu kupatikana na ni vigumu pia kulilinda, lakini linatajwa kuwa ni aina ya penzi bora ambalo ni muafaka kwa maisha ya baadaye ya ndoa kwa wanaopendana. Watu wengi kwa kutotambua aina hii ya mapenzi wamejikuta wakiliharibu kwa kufikiri tu kwamba wapenzi wao wamefika na hivyo kufanya makusudi ya kuharibu misingi ya penzi.

“Nimeshamshika atakwenda wapi, nikikohoa tu anaitika” Kauli kama hizi ni hatari sana katika penzi hili, hivyo inashauriwa ukiona unapendwa na mpenzi wako katika aina hii ya penzi ni vema ukawa macho ili kutolivunja kwa uzembe wako na kudhani unababaikiwa kumbe unapendwa kwa dhati.

No comments:

Post a Comment