Monday, April 29, 2013

Mbowe amtwisha mzigo mzito Zitto

Tabora. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemwagiza Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe kuhakikisha chama kinapata ushindi katika majimbo mengi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mbowe alisema chama chake kitahakikisha kinachukua majimbo ya Samwel Sitta, (Urambo Mashariki), Ismail Aden Rage (Tabora mjini) na Jimbo la Kaliua la Profesa Juma Kapuya, katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Mbowe alimwagiza mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kuhakikisha kwamba majimbo hayo yanachukuliwa na Chadema katika uchaguzi mkuu ujao.
Alimtaka kufanya kampeni za mtaa kwa mtaa, nyumba kwa
hadi nyumba na mtu kwa mtu ili kuhakikisha kwamba wabunge hao wa sasa katika majimbo hayo hawachaguliwi tena na wananchi katika uchaguzi huo.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Town School mjini Tabora, pamoja na mambo mengine alisema anazindua kampeni hiyo kwa ajili ya mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi ambapo Zito Kbwe alikabidhiwa jukumu la kuisimamia  kanda hiyo.
Aliwageukia polisi na kuwataka kukiunga mkono chama hicho ili kikifanikiwa kuingia madarakani kiweze kuwaboreshea mishahara yao kuliko ilivyo sasa akidai wanalipwa mishahara kiduchu ikilinganishwa na ugumu wa kazi yao.
“Nyie makamanda nanyi mmepigika kama sisi, sasa ninachowaomba tuungeni mkono kupambana na hawa CCM ili tuwakomboe wanyonge,” alisema Mbowe.
Awali Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe alisema Kanda ya Magharibi ina historia katika nchi kwa Mkoa wa Tabora kuwa kitovu cha mapambano ya uhuru wa nchi na Kigoma kuwa kitovu cha mapambano ya mageuzi.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment