Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka wa fedha 2013/14, iliyokuwa ipitishwe na Bunge jana, imekwama na kuahirishwa hadi Jumatatu.
Hatua hiyo ilifikiwa, baada ya wabunge kutoridhika na kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya wizara hiyo.
Wakati wabunge hao wakichangia hoja zao katika mjadala wa bajeti hiyo, iliyowasilishwa na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe juzi, walionesha msisitizo kuwa hali ya upatikanaji wa maji ni mbaya nchini.
Mbali na kuelezea hali mbaya ya maji majimboni, wabunge wengine walitoa ushahidi kuwa wanakotoka hulazimika kuoga kwa zamu na wakati mwingine hawaogi kwa siku kadhaa.
Spika wa Bunge, Anne Makinda ndiye aliyeahirisha kupitishwa kwa bajeti hiyo, wakati akitoa majibu ya Mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM).
Nchemba katika hoja yake aliyoombea Mwongozo, alitaka mjadala wa Bajeti hiyo usitishwe, ili kutoa nafasi kwa Serikali kukutana na Kamati ya Bajeti na kuangalia namna ya kutatua ufinyu wa fedha zilizotengwa.
“Naona sasa mahitaji ya wabunge wote na wananchi kwa jumla ni Bajeti hii, kwa kweli iboreshwe, ili ifikie malengo stahiki katika maeneo yetu.
“Ni kweli suala la maji hatuwezi kulifanyia utani, sasa naitaka Wizara ya Maji, Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha, zikafanyie kazi suala hili, walete majibu ya uhakika hapa Jumatatu,” alisema Makinda.
Alisema amefuatilia na kubaini kuwa idadi kubwa ya wabunge waliochangia mjadala huo wa maji, wamekataa kuiunga mkono Bajeti hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kushughulikia suala hilo kwa utaratibu wa majadiliano ambao Bunge hilo limeridhia.
“Tangu jana (juzi) hadi leo (jana), hakuna anayeunga mkono suala hili, mkumbuke utaratibu tuliojianzishia wenyewe wa majadiliano, ni vyema tuliwasilishe kwa Kamati ya Bajeti ili lipatiwe ufumbuzi,” alisisitiza.
Wakati kikao cha Bunge kikianza jana, pamoja na Mwigulu, pia Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), walitaka mjadala huo usitishwe, ili kutoa fursa kwa Serikali kuboresha kiwango cha fedha za Bajeti hiyo.
Juzi na jana wakati wabunge wakichangia mjadala huo, walikataa kuunga mkono Bajeti hiyo huku wakitaka kiwango cha fedha kilichotengwa kwa Wizara hiyo Sh bilioni 398, kiongezwe angalau Sh bilioni 185, ili miradi mingi ya maji hasa vijijini itekelezwe.
Pia katika mjadala huo, baadhi ya wabunge walijikuta wakilumbana kuhusu mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, uliotengewa Sh bilioni 56 ambapo wengine walidai Waziri wa Maji, amejipendelea huku wengine wakitetea hoja hiyo.
Michael Laizer, Mbunge wa Longido (CCM), katika mchango wake, alisema katika jimbo lake wananchi hasa wazazi wanalazimika kuoga kwa zamu, kutokana na shida ya maji na kuiomba Serikali kufuta safari za nje, ili fedha zipelekwe katika miradi ya maji.
Mbunge wa Viti Maalumu Agnes Hokororo (CCM), aliishauri Serikali kuangalia mbinu mpya kwa ajili ya kuboresha miradi ya maji kwa kuwa inaathiri wananchi hususan wanawake.
Alitolea mfano Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kuwa kutokana na ukosefu wa maji, wanawake hufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wanapotafuta maji hayo.
“Nasema wazi hapa, wanawake wa mikoa ya Kusini wanapata shida. Mfano kijiji cha Nanjota, Wilaya ya Masasi, wanawake wanashindwa kushiriki shughuli za maendeleo kwa kuwa wanatumia saa 24 kutafuta maji na wakati mwingine wanarudi bila kuyapata,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili (Chadema), alitaka fedha zilizotengwa katika mradi wa maji wa Mwanga, zigawanywe katika maeneo mengine, ili nako miradi ya maji itekelezwe na wananchi wa maeneo hayo nao wapate maji.
Si kwamba hatupendi maji yaende Mwanga, lakini utaratibu uliotumika si mzuri, haiwezekani Sh bilioni 56 zote ziende Mwanga wakati maeneo mengine kuna shida ya maji,” alisisitiza.
Alieleza kushtushwa na kitendo cha Wizara ya Maji kutoa tangazo la zabuni kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kuhusu mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, wakati Bajeti hiyo haijapita jambo ambalo alidai ni dharau kwa wabunge.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kama alivyofanya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM) kwa kuja na mchoro aliouita nyoka wa shaba, naye aliwasilisha picha halisi zinazoonesha wanawake wanavyopata shida kutafuta maji.
“Namwunga mkono Kangi na mimi naleta picha hii inayoonesha mazingira halisi ya tatizo hili. Mbunge yeyote atakayeunga mkono Bajeti hii, hafai kurudi
bungeni mwaka 2015, naomba mjadala huo uahirishwe ili Bajeti iboreshwe zaidi,” alisisitiza.
bungeni mwaka 2015, naomba mjadala huo uahirishwe ili Bajeti iboreshwe zaidi,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment