KAULI ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, kwamba kuna njama za kumwongezea Rais Jakaya Kikwete, muda wa kuongoza nchi, ni uzushi mtupu na ni upotoshaji usiokuwa na msingi.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu iliyotumwa kwa vyombo vya habari juzi, ilifafanua kwamba Rais Kikwete hafahamu kuwepo mipango hiyo, na kumtaka Profesa Lipumba aisaidie jamii kusema nani anafanya mpango huo, ili ukweli ujulikane.
“Aidha, Mheshimiwa Rais anawasihi wanasiasa na Watanzania kwa ujumla, kuacha tabia za uongo na uzushi na kuwapotezea muda Watanzania kufikiria mambo yasiyokuwepo.
“Ukweli ni kwamba, kama ambavyo amesema mara nyingi, ni matarajio ya Rais Kikwete kuwa mchakato wa Katiba utakamilika mwaka 2014, na kuwezesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika chini ya Katiba Mpya kama inavyotarajiwa ,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Ikulu, Rais Kikwete anatarajia baada ya uchaguzi wa 2015, atapata nafasi ya kustaafu mwisho wa kipindi chake cha uongozi kwa taifa letu.
No comments:
Post a Comment