RASIMU ya Sera ya Elimu na Mafunzo nchini inapendekeza
kuunganisha elimu ya msingi na sekondari ya kawaida ya sasa ili kuunda
elimu-msingi itakayotolewa kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka
2018, imefahamika.
Rasimu
ya kwanza ya Sera hiyo imeshakamilika na sasa wadau mbalimbali wanatoa
mapendekezo yao kuiboresha, kabla ya kupelekwa bungeni ili kutungiwa
sheria.
Aidha,
mikakati hiyo itakayotekelezwa ni kuhuisha muundo na utaratibu mpya wa
elimu na mafunzo kwa kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa miaka
mitatu na mitano anapitia elimu ya awali kwa kipindi kisichopungua
mwaka mmoja kabla ya kujiunga na elimu-msingi.
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alithibitisha kwa
gazeti hili wiki hii mjini hapa kuhusu kukamilika kwa rasimu ya kwanza
ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2013.
“Ni
kweli Sera hiyo imekamilika baada ya kuandaliwa kwa miaka mitatu.
Imepita kwa wadau mbalimbali, mashuleni, vyuoni na katika taasisi
mbalimbali nchini ambao wametoa maoni yao. “Jumapili (kesho)
tunatarajia kuwa waheshimiwa wabunge nao watapata fursa ya kuijadili na
kutoa maoni yao katika semina iliyoandaliwa maalumu kwao,” alisema
Mulugo katika Viwanja vya Bunge.
Alisema
baada ya maoni hao ya wabunge, watapeleka Rasimu hiyo kwa mamlaka
husika kwa ajili ya andiko la mwisho kabla ya kupelekwa katika Bunge
lijalo ili itungwe sheria kuhusu Sera ya Elimu na Mafunzo.
Hata
hivyo, semina hiyo huenda isifanyike kesho kutokana na kuingiliana na
ratiba nyingine, kwani wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watakuwa na
mkutano na Mwenyekiti wao wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kwenye Ukumbi
wa White House mjini hapa.
Wiki
moja iliyopita, wakati akiongoza kikao, Spika wa Bunge, Anne Makinda
aliwaambia wabunge kuwa makabrasha waliyokuwa wakipewa na wahudumu ni
kuhusu Sera ya Elimu na hivyo waende wakayasome, kwani kuna siku
wataijadili.
Kwa
mujibu wa rasimu, mambo mengine yanayotarajiwa kutekelezwa na Sera ni
kuhuisha mitaala ya sasa ya elimu ili ikidhi muundo mpya wa elimu na
mafunzo, kuhuisha sheria na taratibu mbalimbali za utoaji elimu ili
ziendane na muundo mpya wa elimu-msingi.
Kuimarisha
mfumo wa usimamizi, ithibati na udhibiti wa utoaji wa elimu na mafunzo
katika ngazi mbalimbali ili kukidhi malengo na muundo mpya wa
elimu-msingi.
Nyingine
ni kuongeza ubora wa miundombinu katika shule za sasa za msingi ili
kukidhi mahitaji na malengo ya elimu-msingi ikiwa ni pamoja na kuongeza
madarasa ya elimu-msingi katika kila shule ya msingi ya sasa, kujenga
maabara za sayansi na maktaba katika kila shule ya elimu-msingi.
“Kutenga
rasilimali fedha za kutosha kwa ajili ya nyenzo, vifaa na zana za
kufundishia na kujifunzia, vitabu vya kiada na ziada, maandiko,
machapisho ya maktaba pamoja na vifaa vya maabara,” ilieleza rasimi
hiyo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Kuimarisha matumizi ya
lugha za Kiswahili na Kiingereza katika ngazi ya elimu – msingi kama
lugha za kujifunzia na kuwasiliana.
Kuweka
utaratibu utakaohakikisha kuwa wanafunzi wanaomaliza elimu na mafunzo
ngazi husika kwa ufanisi na wale wanaokatisha masomo au mafunzo yao kwa
sababu mbalimbali, wanaendelea na kuhitimu masomo au mafunzo yao
katika mfumo rasmi wa elimu na mafunzo. Jambo jingine litakalotekelezwa
ni kutoa elimu kwa umma kuhusu madhumuni, malengo na matarajio ya Sera
mpya ya Elimu na Mafunzo.
Rasimu ilieleza kuwa mambo chanya yanayotarajiwa kupatikana baada ya mkakati kutekelezwa ni kuwepo kwa elimu ya awali ya lazima kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja kabla ya kujiunga na elimu msingi, kuwepo
kwa elimu msingi ya miaka 10 kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha
nne cha sasa kwa watoto wote wenye rika la kwenda shule.
Matokeo
mengine ni kuwepo kwa mfumo nyumbufu, miundo na taratibu za
kujiendeleza katika mikondo anuai ya kitaalamu na kitaaluma, kuwepo kwa
elimu na mafunzo yenye viwango, ubora na sifa zinazotambulika kitaifa,
kikanda na kimataifa.
“Kuwepo
kwa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo zinazokidhi mahitaji ya
wananchi na ya nchi kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia.
“Kuwepo
kwa ugharimiaji endelevu wa elimu na mafunzo na kuwepo kwa mfumo wa
elimu na mafunzo unaozingatia masuala mtambuka,” ilifafanua Rasimu ya
Sera ya Elimu na Mafunzo.
Kuhusu
elimu ya awali, ilieleza kuwa mkakati ni kuweka vigezo, viwango na
taratibu ili elimu ya awali iwe ya lazima na itolewe katika kila shule
ya elimu – msingi, na kuwa sheria, miongozo na taratibu kuhusu elimu
hiyo lazima kuwekwa na kutekelezwa ifikapo mwaka 2018.
Katika
elimu msingi, ni kuwa ya lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato
cha nne, na kutolewa kwa miaka 10 na umri wa kuanza darasa la kwanza
kuwa kati ya miaka minne hadi sita kulingana na uwezo wa mtoto kumudu
masomo katika ngazi husika.
Shabaha
katika eneo hili ni sheria na miongozo kuhusu elimu-msingi kuwekwa na
kutekelezwa ifikapo mwaka 2016, mpango wa utekelezaji wa utoaji wa
elimu-msingi kuwepo ifikapo mwaka 2018 na elimu-msingi kutolewa ifikapo
2018.
Kwa
mujibu wa dibaji ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa, Sera mpya imeandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau
ikitilia maanani mafanikio yaliyoletwa na Sera zilizotangulia na
kulifanya Taifa kupiga hatua katika nyanja za elimu na mafunzo.
“Sera
kuu zilikuwa ni Sera ya Elimu na Mafunzo 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi
na Mafunzo 1996 na Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu 1999 ambazo
zilitekelewa sambamba na sera nyingine ambazo zinaigusa sekta ya elimu
na mafunzo kama vile Sera ya Sayansi na Teknolojia 1996, Sera ya Habari
na Utangazaji 2003, Sera ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na ya Binafsi
2009 pamoja na nyingine za aina hiyo,” alisema Dk Kawambwa.
No comments:
Post a Comment