POLISI katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikila watu watano kwa tuhuma za kupatikana wakiwa na milipuko hatari.
Akizungumza leo, Kamanda wa Polisi wa
Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika
msako mkali unaoendelea kufanywa na askari polisi katika maeneo ya
Kunduchi jijini humo.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Juma
Khalfani (24), Reuben Patrick (26), Happy Charles (28), Sadick Seif (32)
na Iddi Shaaban (40), wote wakazi wa Kunduchi Mtongani katika Manispaa
ya Kinondoni.
Alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao
kunatokana na taarifa walizozipata kutoka kwa raia wema. Kova alisema
watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na nyaya 62 za milipuko zikiwa
zimefungwa betri, vifaa nane vya kusababisha milipuko, nyaya ndefu
mizunguko minne, 'tube' 20 za urefu wa sentimita 30 zilizojazwa mbolea
ya urea na tambi rola moja.
Alisema katika operesheni hiyo pia
wamefanikiwa kukamata gari lenye namba za usajili T 772 BYC aina ya Noah
pamoja na pikipiki ya miguu mitatu yenye namba T 959 BTE zikiwa kwa
mtuhumiwa Sadick Seif ambae alishindwa kuthibitisha uhalali wa umiliki
wake.
Aidha alisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo
utakapokamilika jalada lake litapelekwa kwa mwanasheria mkuu wa
serikali kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
No comments:
Post a Comment