Monday, May 20, 2013

SUGU AMUUNGA JAYDEE BUNGENI, ASHANGAZWA NA SERIKALI KUWA KIMYA KATIKA MGOGORO WA JAYDEE NA CLOUDS FM.

Waziri Kivuli wa  Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi akisoma hutuba ya kambi ya upinzani hivi punde amesema kwamba baadhi ya vyombo vya habari vikiwamo vituo vya redio vimekuwa vikiwanyonya wasanii nchini na kusababisha kuwa maskini.

Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema bungeni kwamba hivi sasa kuna mgogoro mkubwa kati ya Lady Jay Dee na Radio Clouds FM, lakini serikali imekaa kimya mpaka sasa.

"Serikali imekaa kimya haitatui matatizo ya wasanii, hivi leo Clouds FM haipigi muziki wa Lady Jay Dee, tunakwenda wapi, chama cha wasanii ambacho ni halali
kimetaifishwa na kuundwa kampuni ya kusimamia shughuli za wasanii, lakini kwa malengo ya kuwanyonya," amesema Sugu.

Kutokana na mgogoro unaoendelea kati ya Lad Jaydee na Clouds FM, Sugu ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini amewataka wasanii Tanzania kuacha uwoga na kutetea haki zao.

Ameitaka serikali kuchukua hatua ya kuwatetea wasanii na iache kuwatumia kwa maslahi yao binafsi. Sugu akihitimisha hutuba yake, amelieleza Bunge kwamba Lady Jay Dee anatimiza miaka 13 tangu aanze muziki na kwamba atafanya tamasha kubwa jijini Dar es  Salaam ambalo litafanyika Mei 31, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

"Kabla sijaitimisha napenda kuwaambia kwamba Jay Dee atafanya tamasha la kusherekea miaka 13 tangu aanze muziki hivyo dada napenda kukuhakikishia kwamba tutakuwa pamoja pale Dar es Salaam," Sugu amesema hivi punde bungeni.

Sugu amemaliza kusoma hutuba ya kambi ya upinzani na sasa wabunge wameanza kuchangia.

credit www.habarimasai.com


No comments:

Post a Comment