Saturday, May 18, 2013

SKENDO: SISTA FEKI WA KIKATOLIKI ANASWA KANISANI....AISHI NDANI YA NYUMBA YA MASISTA BILA KUJULIKANA...!!


AMA kweli dunia inazidi kwenda ukingoni! Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Phyllis Wanjiru Kamau (44), raia wa Kenya amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kwa madai ya kujifanya mtawa wa Kanisa Katoliki na alikuwa akiishi kwenye nyumba za watawa wa kanisa hilo zilizopo Ipogolo mjini hapa.
Tukio hilo lililowashangaza polisi, lilijiri Mei 13, 2013  ambapo baada ya kuwekwa chini ya ulinzi na kumpekua, polisi walimkuta na ‘dokumenti’ zilizozidi kutia shaka.
Sista Wanjiru alikamatwa na jeshi hilo kufuatia masista wenzake orijino kubaini kuwa yeye si miongoni mwa watawa kwa ki-Katoliki kwa sababu ya kushindwa kuishi maisha ya kitawa ndani ya nyumba.
“Sisi tulimpokea tukiamini ni mwenzetu, lakini kadiri tulivyokuwa tukiishi naye, alionekana siye. Masista wa Katoliki tunajuana kwa vitendo hata kama atakuwa anatokea nchi nyingine,” alisema mtawa mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Mtoa habari huyo alisema ukiachilia mbali kukiuka maisha ya kitawa lakini pia Wanjiru alionekana ni msiri kwa mambo mengi aliyokuwa akiyafanya, hali iliyozidi kuwapa wasiwasi wenzake.


“Mambo yake mengi yalionekana  ni ya sirisiri, hakuwa muwazi wa maisha yake ya nyuma wala kuanika historia yake kama wengine tunavyofanya. Alitia wasiwasi hata shule aliyosoma,” alisema sista huyo.



Habari zinadai baada ya masista ndani ya mjengo kumshtukia Wanjiru, walikwenda kuripoti polisi wakitaka mwenzao huyo akamatwe na kukaguliwa kwa umakini ili kuonesha uhalali wa utawa wake na uraia wa Tanzania.
Ndipo polisi walipomzukia na kumweka mtu kati ambapo awali alikiri yeye ni sista lakini baada ya kukaguliwa na kubanwa sana alionekana ni sista feki na pia si raia wa Bongo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, Afande Michael Kamuhanda alipoongea na paparazi wetu aliweka wazi kuhusu sista huyo.
Alisema kabila la mwanamke huyo ni Muwembu kutoka nchini Kenya na alikiri kuwa alidakwa na polisi akiwa katika nyumba za masista zilizopo Ipogolo mjini Iringa.
Aliongeza kuwa baada ya kumtia mikononi, mwanamke huyo aligoma katakata kutoa maelezo ya kina juu ya uingiaji wake nchini Tanzania licha ya kwamba nchi aliyotokea ipo Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ilivyo Tanzania. Nchi nyingine zilizopo kwenye jumuiya hiyo ni Uganda, Rwanda na Burundi.
Kamanda Kamuhanda akaendelea kusema kuwa wakati wa kumpekua Wanjiru walifanikiwa kumkuta na baadhi ya laini za simu za makampuni mbalimbali ya simu ya ndani na nje ya Tanzania.
Mbali na laini za simu, pia alikuwa na hati za kusafiria (passport) mbili, moja ikiwa ni ya Afrika Mashariki yenye namba Ke. 020659 huku hati ya nyingine ikiwa na ya Kenya yenye namba A. 1790366.
Afande huyo akizidi kumuanika sista Wanjiru alisema katika hati hizo, ilionesha kuwa alitembelea Rwanda, Uganda na Tanzania ambapo siku za hivi karibuni alikuwa wilayani Tarime Mkoa wa wa Mara.
Katika hali ya kushangaza, akiwa anahojiwa sista huyo alianguka kama mtu mwenye ugonjwa wa kifafa, jambo linalowawia vigumu polisi kupata maelezo ya kina dhidi ya dhamira yake ya kuingia Bongo.
Kamuhanda ameitaka jamii kuwa makini na wageni mbalimbali, huku akiwaasa kuacha tabia ya kuwaamini watu kwa muonekano wao, kutokana na mwanamke huyo kutumia njia hiyo ambayo inamfanya kila mtu kumuamini.

No comments:

Post a Comment