Saturday, May 18, 2013

HOFU YATANDA BUNGENI KUTOKANA NA TETESI ZA SHAMBULIO LA KIGAIDI MJINI DODOMA




Hali ya wasiwasi imelikumba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuwepo kwa tetesi ya shambulio la kigaidi katika maeneo ya Bunge.


Hali hiyo inafuatia ujumbe mfupi wa maneno uliosambazwa, ukitaadharisha kuwa kuna tukio la kigaidi limepangwa kufanywa katika eneo la Bunge.

Ujumbe huo uliosambazwa kwenye simu za baadhi ya wabunge ulisomeka hivi:-

"Kuna kikundi kina mkakati wa kufanya shambulio la bomu bungeni Dodoma na msikiti wa Msavu Morogoro. Ni ndani ya muda mfupi wakati bado vikao vya Bunge,"ailisema sehemu ya ujumbe huo.


Habari zaidi zinasema kuwa tayari jeshi la polisi imefanikiwa kupata mtu aliyetuma ujumbe huo, ambaye anadaiwa kutuma kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini na wamefanikiwa kumleta mjini hapa kwa mahojiano zaidi ili kufanikisha upelelezi.



Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Mussa Azzan Zungu, juzi alilitangazia Bunge hali hiyo ya hatari  wakati wabunge wakiendelea na mjadala wa hotuba ya makadirio ya matumizi wizara ya Uchukuzi ya mwaka 2013/14, na kulazimika kurudia tangazo hilo wakati akiharisha Bunge.
 


“Waheshimiwa wabunge wote mnaombwa kuanzia kesho tarehe 17, mwezi huu, mwaka huu, kutoegesha magari yenu pembezoni mwa uzio unaozunguka ofisi ya bunge hapa Dodoma…Badala yake magari hayo yaingizwe katika geti la eneo la maegesho ya waheshimiwa wabunge ndani ya viwanja vya Bunge” alisema Zungu


Alisema mbunge yeyote atakaye taka kuegesha gari lake nje ya ofisi, anaombwa aegeshe ng’ambo ya upande wa kaskazini wa barabara itokayo jijini Dar es Salaam.


Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema ulinzi umeimarishwa katika eneo lote la Bunge kuhakikisha hakuna chochote cha hatari kinachoweza kutokea.

“Vijana wangu wanafanya kazi yao vyema na iwapo kuna tishio lolote lile litafanyiwa kazi,” alisema Dk Nchimbi

Dk Nchimbi alisema ulinzi utaendelea kuimarishwa katika eneo hilo kuliko wakati wowote ambao Bunge limewahi kuwekwa katika usalama.

No comments:

Post a Comment