Friday, May 17, 2013

WASANII WAFAFANUA AINA ZA RUSHWA KWENYE MUZIKI
BAADHI ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya wafafanua aina za rushwa zinazotokea katika tasnia ya muziki ambazo zinasababisha kudidimiza muziki pamoja na vipaji vya wasanii.

Rushwa hizo ambazo zinatolewa na baadhi ya wasanii kwa baadhi ya vyombo vya habari kwa ajili ya kupiga muziki wa msanii hata kama hauna sifa,imezidi kuchukua sura mpya kwa kuhusisha baadhi ya mashabiki kwa ajili ya kuomba nyimbo katika radio.

Akifafanua aina ya rushwa hizo jijini Dar es Salaam Hugoline Martin 'Dj Choka' ambaye pia ni mmiliki wa mtandao wa Bongo Star alisema, kuna aina mbili za rushwa ambapo moja ilikuwa imezoeleka kwa wasanii kutoa hela kwa baadhi ya watangazaji wa redio ili kuwezesha nyimbo zao kupigwa kwenye vipindi ambapo rushwa hii imezoeleka kwa baadhi ya wasanii walio wengi nchini.


Kutokana na hali hiyo alisema muziki wa bongo fleva unakuwa kwa kusikilizwa kwa wingi kwenye baadhi ya vyombo vya habari huku ukiwa unakosa sifa ya ubunifu hali inayochangia kufanana kwa baadhi ya nyimbo kuanzia melody hadi mahudhuhi ya nyimbo.

Alisema kuwa rushwa ya aina ya pili  ni ile ya mashabiki ambao wanapewa hela na baadhi ya wasanii kwa ajili ya kuomba nyimbo redioni hali ambayo inaonyesha msanii fulani nyimbo yake kuombwa mara kwa mara hata kama haina sifa na imekosa ubunifu.

"Kuna rushwa nyingi sana kwenye muziki sasa kuna hii mpya ya baadhi ya wasanii kutoa hela kwa mashabiki wao ili kuomba nyimbo kwenye redio kwahiyo utaona nyimbo inaombwa sana hata kama haina sifa hii inasababisha kuushusha muziki wetu " alisema Choka

Akielezea kwa upande wake jinsi anavyofanya kazi na wasanii hao wa muziki wa bongo fleva alisema, ameweka vigezo kwa wasanii hivyo haweki nyimbo ambayo haina vigezo kwenye mtandao wake.

"Nimeshakataa kupigiwa simu na wasanii kuniomba niweke nyimbo yake kwenye mtandao wangu na mimi sipokei hela teyari wanafahamu hilo hivyo muziki ninaouweka kwenye blog ni ule wenye sifa na vigezo tu na siyo kwa ajili ya hela " alisema Choka

Kwa upande wake msanii wa bongo fleva kutoka kundi la TMK wanaume Amani Temba anayejulikana kwa jina la  'Mheshimiwa Temba' amesema kunatofauti kwa upande wa muziki kwa kipindi hiki na kipindi cha zamani ambapo hapo mwanzo muziki ulikuwa unasikika kwa nguvu ya prodjuza pamoja na msanii mwenyewe.

Alisema rushwa imejaa kwenye baadhi ya vyombo vya habari ambapo msanii nyimbo yake haipigwi mpaka atoe hela sababu inayosababisha kuwa na nyimbo nyingi kusikika redioni huku zikikosa sifa ya kuwa nyimbo bora .