Hivi karibuni wanamuziki wa kizazi kipya, wameibua malalamiko kwa waliokuwa mapromota katika shughuli za muziki.
Kimsingi kinacholalamikiwa ni kunyonya au kuingiliwa katika kazi zao za muziki.
Nisingependa kujiingiza kwa undani kwenye
malalamiko hayo, lakini kama mpenzi wa muziki wa Tanzania nimeona kuna
haja ya kuangalia hatima ya muziki huu ikiwa ni pamoja na maendeleo ya
wanamuziki wenyewe.
Kwanza niseme kwamba malalamiko yanayowakilisha kilio cha wanamuziki wengi nchini yanaweza kuwa chanzo cha muziki wetu kudumaa.
Tukubali kwamba fani ya muziki nchini iko katika
hali mbaya, hasa kwa kuwa wanamuziki wengi ni maskini kwani hawafaidiki
na sanaa yao. Tatizo lililopo ni mfumo mbovu wa kuwawezesha wasanii hao
kujitegemea kiuchumi.
Tukiangalia maendeleo ya muziki tangu wakati wa
kupata uhuru mwaka 1961, tunaona mabadiliko mengi ya kisiasa
yaliyofanywa na Mwalimu Julius Nyerere katika uongozi wake, yaliathiri
pia fani ya muziki nchini.
Mkakati wa Mwalimu Nyerere kuunda Serikali dola inayomiliki kila kitu, kuliwanyima uhuru wasanii wengi wa muziki.
Kwa hali hiyo bendi nyingi zikabaki kumilikiw na
mashirika ya umma. Mfano ni Bima Lee Orchestra iliyokuwa chini ya
Shirika la Bima, DDC Mlimani Park iliyokuwa chini ya Shirika la
Maendeleo la Dar es Salaam, Nuta, Juwata na baadaye OTTU ilikuwa
ikimilikiwa na Jumuiya ya Wafanyakazi nchini, na nyinginezo nyingi.
Kutokana na hali hiyo, wanamuziki walikuwa
wakitegemea kulipwa mishahara kila mwezi kama wafanyakazi wengine wa
mashirika hayo. Hawakuwa na mikakati binafsi ya kujiongezea kipato nje
ya mashirika hayo. Haishangazi kuona kuwa muziki wa dansi uliokuwa
ukitamba miaka ya 1970/80 na 90 mwanzoni ulidumaa na kushindwa kuvuka
mipaka ya nchi.
Baadhi ya wanamuziki hawakuridhika na hali hiyo,
wakakimbilia Nairobi Kenya kutafuta maisha. Wapo kina John Ngereza, Issa
Juma, Joseph Just, Mohammed Tika Abdallah Victor Boniface walioungana
na wanamuziki wa Kenya kuunda Kundi la Les Wanyika.
Wengine ni pamoja na Mbaraka Mwinshehe na bendi
yake ya Super Volcano, aliyependelea kurekodi nyimbo zake Nairobi.
Wengine walikwenda huko, lakini hawakuvuna na walirudi tena nchini.
Baada ya kuanguka kwa mfumo wa Ujamaa na
Kujitegemea ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere, bendi hizo nyingi zikaanza
kujitegemea. Lakini hazikufika mbali kwani wanamuziki wengi walikuwa
wamezeeka huku muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva) ukiibuka kwa kasi.
No comments:
Post a Comment