Hiki ni kipande cha hotuba ya kambi rasmi ya upinzani bungeni,iliyo SABABISHA BUNGE KUAHIRISHAASUBUHI,Isome na uielewe
MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O. MBILINYI (MB)
KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA YA HABARI, VIJANA,
UTAMADUNI NA MICHEZO KWA MWAKA
WA FEDHA 2013/2014
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya
kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013)
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Dira ya Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo ni “kuwa na taifa
lililohabarishwa vizuri, lina vijana wenye
uwezo na malezi bora, linathamini
utamaduni wake na linakuwa mahiri
katika michezo ifikapo mwaka 2025.”
Aidha, ‘dhamira’ ya wizara hii ni
‘kuendeleza utambulisho wa taifa kwa
kuwezesha upatikanaji mzuri wa habari,
kuwawezesha vijana kiuchumi na
kukuza utamaduni na michezo kwa
umma kwa maendeleo ya kijamii na
kiuchumi.’
Mheshimiwa Spika,
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Serikali hii ya CCM imeshindwa
kutekeleza dira na dhamira iliyotajwa
katika maandiko ya kisera ya Wizara.
Badala yake, chini ya usimamizi wa
Wizara hii, Tanzania imegeuka kuwa
taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri
juu ya matendo ya watawala. Tanzania
imegeuka kuwa taifa linalofungia
magazeti yanayofichua ufisadi, uchafu
na matumizi mabaya ya madaraka
miongoni mwa viongozi, watendaji na
watumishi wa Serikali hii ya CCM.
Tanzania imegeuka, chini ya usimamizi
wa Wizara na Serikali hii ya CCM, kuwa
taifa linaloteka nyara wanahabari,
kuwatesa kwa kuwang’oa kucha na
meno, kuwatoboa macho, kuwamwagia
tindikali na hata kuwaua. Tanzania sio
nchi inayoandaa vijana wake tena.
Haiwapi tena elimu bora wala kuwapatia
maarifa, uwezo na malezi bora; ni nchi
isiyowawezesha wala kuwathamini vijana
wake; ni nchi inayoruhusu vijana wake
kunyonywa na kutoendelezwa; na ni
taifa ambalo limeachia utamaduni
utambulisho wake kama taifa kupotea
kabisa. Aidha, katika fani ya michezo ya
aina zote, Tanzania imeporomoka kutoka
taifa lililokuwa linaheshimika kimataifa
katika miaka ya sabini na kuwa
alichokiita rais mstaafu Ali Hassan
Mwinyi, ‘kichwa cha mwendawazimu’
ambacho kila kinyozi anajifunzia
kunyolea!
2. UHURU WA UHARIRI NA USALAMA WA
WANAHABARI
Mheshimiwa Spika,
Kwa masikitiko makubwa, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inalitaarifu Bunge
lako tukufu kwamba sasa Tanzania
imeingia rasmi katika orodha ya fedheha
(The List of Shame) ya mataifa ambayo
taaluma ya habari ni taaluma ya hatari
kwa wale wote wanaoitumia kama
sehemu ya wajibu wao kwa taifa na
kama ajira yao. Kwa mujibu wa taarifa ya
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari
Ulimwenguni (the Committee to Protect
Journalists - CPJ) iliyotolewa mwaka huu
2013, kwa mara ya kwanza tangu
kuanzishwa kwa CPJ mwaka 1992,
Tanzania imeingizwa kwenye orodha ya
nchi 20 ambazo ni hatari kwa waandishi
wa habari kufanya kazi zao kutokana na
hatari ya kuuwawa kwa mwaka 2012 (20
Deadliest Countries in 2012). Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, ilishikilia nafasi
ya 7 ulimwenguni kati ya nchi 20
zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha
ya waandishi wa habari.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, tishio
kubwa kwa waandishi wa habari duniani
ni kuuwawa kwa kutekwa na kuteswa
na/au kutishiwa maisha. Aidha, Serikali
na vyombo vyake vya ulinzi na usalama
ni washiriki wakubwa wa mauaji ya
waandishi wa habari. Kwa mujibu wa
takwimu za CPJ, kati ya waandishi
waliouwawa mwaka 2012, karibu ya 20%
waliuwawa ama na maafisa wa serikali
au na majeshi yake. Karibu idadi hiyo
hiyo ya waandishi wa habari waliuawa
kwa sababu ya kufuatilia taarifa za
kiuchunguzi na za hatari. Taarifa hiyo
inaonyesha kwamba hadi kufikia Aprili
2013, waandishi wa habari wapatao 30
tayari wamekwishauawa ulimwenguni
wakati wakitimiza wajibu wao; wakati
mwaka 2012 waandishi wa habari 103
waliuwawa ulimwenguni kote.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya CPJ inaungwa mkono na
ushahidi wa matukio mengi
yanayodhihirisha kwamba maisha ya
waandishi wa habari wa Tanzania yako
hatarini kutokana na vitendo na vitisho
kutoka kwa Serikali na watendaji wake
ambao hawataki kusikia ukweli dhidi yao
ukianikwa hadharani. Kudhihirisha kauli
hii tunaomba kumnukuu mwanahabari
mahiri na mmoja wa wahanga wa vita
dhidi ya wanahabari na uhuru wa habari
hapa nchini, Mzee Ndimara
Tegambwage:
“Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi
wa jiji la Mwanza, walikusanywa na
wenye uwezo kufanya maandamano
makubwa kwa walichoita ‘kupinga
mwandishi Richard Mgamba kuandika
uongo’ na kudai kwamba alikuwa
Mkenya na ‘siyo raia wa Tanzania.’
Desemba 2009, mwandishi Frederick
Katulanda wa Mwanza, alivamiwa
nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza
sauti na kudai kuwa ana nyaraka za
akaunti za benki za Halmashauri ya Jiji la
Mwanza. Walikuwa na mapanga.
Walikuwa wakichagizana kwa kusema,
“Kata kichwa! Kata kichwa!” Waliondoka
na mafaili. Walimwachia kilema mguuni
na makovu mikononi.
“Mwezi Septemba, 2010 wakati wa
kampeni za Uchaguzi Mkuu, katika eneo
la Nyambiti, Jimbo la Sumve wilayani
Kwimba, mkoani Mwanza, mwandishi
Frederick Katulanda alivamiwa na
kupigwa na watu wapatao 15 waliojiita
“Green Guard” - wa “chama cha kijani.”
Katika “kumshughulikia,” Katulanda
anasema, walikuwa wakionyesha kuwa
na ujuzi mkubwa wa judo na karate
huku wakidai kuwa anawaandika
‘vibaya’ Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mwaka 2011 mwandishi Richard
Massatu alikutwa amekufa katika eneo la
Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari
viliripoti kuwa macho yake yalikuwa
yametobolewa na kuwekwa gundi aina
ya super glue; mguu wa kushoto na
mbavu vilikuwa vimevunjika. Vyombo
vya habari viliripoti kuwa Massatu
aliyekuwa mmiliki na mhariri mkuu wa
gazeti la Kasi Mpya (sauti ya umma),
alionekana mara ya mwisho usiku wa
kifo chake akiwa na maofisa wa polisi na
usalama katika baa iitwayo Cross Park
katika eneo la Igoma.
“Tarehe 3 Januari, maiti ya mwandishi
Issa Ngumba iliokotwa katika pori la
mlima Kajuruheta, kijiji cha Mhange,
wilayani Kakonko katika mkoa wa
Kigoma.Ngumba alikuwa mwandishi wa
habari wa Redio Kwizela. Tangu mwezi
uliopita Machi, mwandishi wa habari
Erick Kabendera anayeishi Dar es
Salaam, anaishi kwa wasiwasi. Wazazi
wake waishio Bukoba, wamehojiwa na
‘ofisa usalama’ kwa kile kilichoitwa
‘uhalali wa uraia wao.’
“Kuuwawa kwa aliyekuwa mwandishi wa
habari wa Kituo cha Luninga cha ITV,
John Lubungo ambaye alikuwa mfuatiliaji
mahiri wa habari zinazohusu
wafanyabiashara au biashara haramu ya
dawa za kulevya ambayo inadaiwa
kufanywa na watu wakubwa nchini,
wakiwemo vigogo serikalini. Kuna orodha
ndefu ya waandishi wa habari
waliotishwa na wanaoendelea kutishwa;
waliopigwa na polisi na askari magereza
(Ukonga, Dar es Salaama) kwa tuhuma
mbalimbali; waliotishiwa maisha kwa
simu na hata kwa kufuatiliwa na watu
wasiowafahamu.”
Kwa sababu ya uadilifu na kutopenda
kujikweza, Mzee Tegambwage hakutaja
shambulio la tindikali na mapanga dhidi
yake na mwandishi mwenzake Saed
Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi,
ambalo baadae lilifungiwa na Serikali hii
ya CCM.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake wakati wa mjadala wa
bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya
tarehe 3 Mei mwaka huu, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni ilielezea kwa kirefu
jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM
imekuwa tishio kwa maisha ya waandishi
wa habari na kwa uhuru wa habari katika
nchi yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ilirejeaRipoti ya Timu Maalum
ya Uchunguzi Iliyoteuliwa na Baraza la
Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) Kuchunguza
Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa
Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi
Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha
Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani
Iringa, iliyotolewa na Baraza la Habari
Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), taasisi mbili huru
zinazojihusisha na masuala ya habari
Tanzania.
Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF,
matokeo ya uchunguzi wao “...
yanadhihirisha bila wasi wasi kwamba
polisi kwa makusudi waliwavurumisha
waandishi waliotoka Iringa wakati
wakikusanya habari za shughuli za
CHADEMA katika kijiji cha Nyololo. Zaidi
ya hapo, Daudi Mwangosi mwenyewe
aliuawa akiwa mikononi mwa polisi huku
wakisimamiwa moja kwa moja na
Kamanda (wa Polisi wa Mkoa wa Iringa
SACP Michael) Kamuhanda.” Ripoti hiyo
inaelezea jinsi Marehemu Mwangosi
alivyouawa: “Alipoangalia nyuma, Daudi
Mwangosi aliona kikundi cha polisi
wakimpiga mwandishi mkuu wa gazeti la
Nipashe wa Iringa, Godfrey Mushi....
Wakati mwandishi Godfrey Mushi akiwa
bado anapigwa na polisi, marehemu
Mwangosi aliwakimbilia akiwaomba
waache kumdhuru zaidi Mushi kwa kuwa
alikuwa mwandishi tu. Polisi
hawakumsikiliza. Badala yake
wakamburuta mwandishi huyo ambaye
tayari alikuwa amepoteza fahamu na
kumweka kwenye gari lao na
wakamgeukia Daudi Mwangosi
mwenyewe, wakampiga kwa nguvu
mpaka akapoteza fahamu.”
Hata amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi
Mafinga Mwampamba kuwataka askari
polisi waache kumpiga marehemu
Mwangosi haikusikilizwa na askari hao. Ili
kujiokoa, marehemu Mwangosi
alimkumbatia OCS Mwampamba na
“baadaye kumwangukia miguuni mwake
kuepuka kipigo zaidi.” Kwa mujibu wa
Ripoti ya MCT/TEF, “picha za mgando
zinaonyesha polisi mmoja akipiga bomu
la machozi tumboni mwa marehemu
Mwangosi kwa karibu kabisa.” Bomu hilo
liliusambaratisha mwili wa marehemu
Mwangosi aliyekufa papo hapo. Kwa
sababu marehemu Mwangosi alikuwa
chini ya miguu ya OCS Mwampamba,
“naye pia alijeruhiwa vibaya.”
Mheshimiwa Spika,
Sio MCT/TEF pekee zilizofanya uchunguzi
wa mauaji ya Marehemu Mwangosi.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora nayo ilitoa Taarifa ya Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora ya
Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea Kifo
cha Daudi Mwangosi Kilichotokea
Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo,
iliyobaini kwamba Marehemu Mwangosi
“... alizingirwa na askari, aliteswa na
hatimaye ... alipigwa bomu na kufa papo
hapo.” Aidha, kwa mujibu wa Taarifa
hiyo, “... Tume imejiridhisha kuwa tukio
la lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi
limegubikwa na uvunjwaji wa haki za
binadamu na ukiukwaji wa misingi ya
utawala bora.” Taarifa ya Tume
inafafanua kuwa, “... Tume imejiridhisha
kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki ... ya
kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa,
haki ya usawa mbele ya sheria na haki
ya kukusanyika na kutoa maoni.”
Mheshimiwa Spika,
source page ya kiroho safi [fb]
No comments:
Post a Comment