Saturday, May 18, 2013

TANGA: MAKANISA MAWILI YACHOMWA MOTO....


Makanisa mawili yamechomwa moto usiku wa kuamkia leo huku bila mafanikio watu wasiofahamika wakijaribu kuteketeza kwa moto banda moja la kuoneshea picha za video.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alisema tukio la kwanza lililotokea majira ya saa 8 usiku katika Kanisa la Betham lililoko eneo la Donge ambapo wahusika waliteketeza kwa moto jengo la Kanisa dogo lililokuwa likitumika zamani na kisha kuingia ndani ya Kanisa kubwa la sasa na kuviwasha kwa moto vitambaa vilivyokuwa vimefunika madhabahu.

Massawe alisema:


Kanisa lililoteketezwa hapo lilikuwa la zamani ila sasa linatumiwa na waumini wa Betham kwa ajili ya kufundisha watoto lakini ibada zote zinafanywa kwenye jengo hilo jipya ambalo ndilo lililochomwa vitambaa vilivyokuwa vimefunika madhabahu.

Aidha, alisema taarifa za kuchomwa Kanisa hilo zilitolewa na Sauli Taminola mmoja wa waumini hao ambaye analala hapo Kanisani ambaye anadai alishtuka kutoka usingizini mara baada ya kuona moto ukiwaka madhabahuni ndani ya Kanisa.

Tukio jingine la usiku huo huo alisema liliripotiwa kuhusisha Kanisa la Miracle Revival lililopo eneo la Makorora majira ya saa 9 za usiku ambapo watu walidai walishituka usingizini na kuona moto ukiwaka kwenye nguzo za Kanisa hilo ndipo wakapiga kelele za kuomba msaada.

Mchungaji ambae anaishi jirani na kanisa alisema aliona watu wakiwasha moto magurudumu (matairi) ya baiskeli na kuyafunga kweney boriti za kanisa ili ziweze kuungua moto lakini baada ya kuwakurupusha jaribio hilo lilishindwa kwakuwa moto ulidhibitiwa na watu pasipo kuleta madhara makubwa
alisema Kamanda Massawe.

Akizungumzia klabu ya pombe za kienyeji iliyoteketea usiku huo alisema tukio hilo lilitokea katika eneo la Kwanjeka kwenye baa inayofahamika kama ‘Bongola’ na kudai kwamba chanzo ni shoti ya umeme.

Kamanda Massawe alisema tukio la nne limehusisha banda moja la kuoneshea mikada ya picha za video huko huko Kwanjeka ambalo nalo lilikaka kuteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana lakini jaribio lao halikufanikiwa.


No comments:

Post a Comment