Monday, May 13, 2013

Matokeo mtihani wa kidato cha nne kutangazwa wiki hii


Matokeo mapya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 yanatarajia kutangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi siku yeyote wiki hii. 

Kutangazwa upya kwa matokeo hayo kunafuatia uamuzi uliochukuliwa na serikali hivi karibuni kufuta wa matokeo hayo ili yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011. 

Habari ambazo NIPASHE imezipata jana na kuthibitishwa na 
viongozi wandamizi wa wizara hiyo, kazi ya kufanya marekebisho ya matokeo hayo imeshakamilika na yatatangazwa wiki hii. 
“Kazi ya kuandaa matokeo imekwishakamilika sababu ni kazi inayofanywa na watu watatu kwa kutumia kompyuta,” alisema ofisa mmoja ambaye alisema taarifa rasmi zitatolewa na Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
 
Dk. Kawambwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),  Dk. Joyce Ndalichako, walipotafutwa kueleza suala hilo jana, simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa. 
Hata Hivyo, Afisa Habari wa Necta, John Nchimbi, alisema mchakato wa kuandaa matokeo hayo unaendelea na kwamba yatatangazwa muda wowote. 
Mei 3, mwaka huu serikali ilitangaza kufuta matokeo hayo na kuamua yaandaliwe upya. 




Uamuzi huo wa Serikali ambao ulitangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kwamba umetokana na matokeo mabaya ya mitihani huo yaliyosababisha zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi kupata sifuri. 
Kutokana na matokeo hayo, Serikali iliunda Tume inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza matokeo hayo ili kupata ufumbuzi wa kudumu. 
Katika mtihani wa mwaka 2012, wanafunzi 367,756 walifanya mtihani huo na waliofaulu ni 126,847. Waliofaulu kwa kwa madaraja ya kwanza hadi la tatu ni 23,520 sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327 sawa na asilimia 28.1, huku 240,909 ambao ni asilimia 65.5 wakipata daraja sifuri.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment