HATIMAYE Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa kampuni ya Clouds Media Group ya jijini Dar es Salaam, Ruge Mutahaba, amefungua kesi ya madai dhidi ya mwanamuziki nguli, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, ambayo inataanza kusikilizwa Mei 27 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Kupitia kwa wakili wake, Ruge amefungua madai dhidi ya Jay Dee kupitia jalada namba 29/2013 chini ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Athuman Nyamlani, ambaye pia ni Makamu wa Rais Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Hata hivyo, wakili wa Ruge ambaye alikuwa mahakamani hapo hakuwa tayari kudokeza madai ya msingi ya mashtaka yaliyofunguliwa ingawa pande hizo mbili zimekuwa kwenye malumbano ya maneno ambapo msanii huyo alidai Clouds Media Group imekuwa hairushi matangazo ya bendi yake.
“Tumefungua kesi ya madai, zaidi mumtafute Jay Dee mwenyewe au Ruge ndiyo wenye kuongelea; mimi siwezi kuongea chochote hadi nitakaporuhusiwa na mteja wangu,” alisema wakili huyo ambaye hata jina lake alikataa kuweka hadharani.
Awali mwandishi wa habari hizi aliweza kuwasiliana na Gadna G Habash ambaye ni Meneja na Mume wa Mwanamuziki Lady Jay Dee, aliyekiri kupokea taarifa ya kuitwa mahakamani kwa Jay Dee, ingawa hajui kwa ajili ya nini.
“Ni kweli walifika watu na barua ambayo ni ya wito kwa Jay Dee ili afike mahakama ya Kinondoni, Jumatatu (jana); hata hivyo hawakumkuta, lakini wito huo amefikishiwa mlengwa,” alisema Gadna.
Gadna alisema hajajua Lady Jay Dee anaitiwa nini na amemwelezea na amesema atatekeleza wito huo. Hata hivyo, wakati tunakwenda mitamboni, kulikuwa na habari kuwa Gadna na Jaydee walifika mahakamni majira ya saa sita mchana.
No comments:
Post a Comment