MAGAZETI yanayochapisha picha zenye kukiuka maadili hususan za wanawake kwa kuwageuza malighafi ya kujiingizia kipato, yamemulikwa bungeni huku Serikali ikihojiwa sababu za kutoyachukulia hatua.
Mbunge wa Konde, Khatib Saidi Haji (CUF) alihoji hayo kwenye swali la nyongeza baada ya kujibiwa swali la msingi ambalo alitaka kufahamu ni aina gani ya makosa yanaweza kusababisha Serikali kuyafungia magazeti kama ilivyotokea kwa gazeti la Mwanahalisi.
Katika majibu ya msingi, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla alitaja sababu mbalimbali za kufungia magazeti ikiwa ni pamoja na yanayochapisha habari zisizo za ukweli, habari za uchochezi na kuchapisha picha mbaya zinazokiuka maadili ya Mtanzania na magazeti yanayokiuka taaluma ya habari.
Sababu nyingine ni pamoja na gazeti kutochapishwa kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kufilisika kwa kampuni inayochapisha magazeti husika.
Licha ya mbunge huyo kushutumu magazeti hayo yanayochapisha picha mbaya za wanawake kutofungiwa, pia alilaumu Serikali akisema inatumia sheria dhaifu kudhibiti uhuru wa habari. Alisema sifa za serikali za kidikteta ni kupenda kusifiwa na kutukuzwa.
Naibu Waziri Makalla alisema Tanzania si nchi ya kidikteta kwani inaheshimu uhuru wa wananchi kupata habari.
Alisema kwa msingi huo, ndiyo maana ni miongoni mwa nchi zenye magazeti mengi. Kwa mujibu wa Naibu Waziri, yapo magazeti 52 yanayochapishwa kwa wiki na magazeti 13 ya kila siku.
Alisema uamuzi wa Waziri kufungia magazeti ni wa kisheria na si kwa hisia zake. Kuhusu uwepo wa magazeti yanayochapisha picha chafu, Makalla alisema wizara imepokea changamoto.
Alionya magazeti kwa kusema serikali itachukua hatua itakapothibitika yanakiuka maadili na sheria.
Wakati huo huo akijibu swali la Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa, aliyetaka kufahamu ni lini Sheria ya Vyombo vya Habari italetwa bungeni, Makalla alisema kwa sasa iko ngazi ya Baraza la Mawaziri na wakati wowote itawasilishwa bungeni.
No comments:
Post a Comment