Wednesday, May 15, 2013

HATIMAYE KINYWAJI CHA SODA CHAPIGWA MARUFUKU

SODA.jpg

*Yakatazwa shuleni, watoto chini ya miaka 12
*Sasa yabainika kuwa ina sumu inayoua taratibu
*Yagundulika kupumbaza na kusababisha uteja

SIKU chache baada ya gazeti la Mtanzania kuripoti madhara yanayosababishwa na kinywaji aina ya soda, katika utafiti wake gazeti hilo limebaini mengine mapya.
Kwa mujibu wa utafiti huo, imebainika kuwa soda imepigwa marufuku kutumiwa na watoto walio na umri chini ya miaka 12 na walio shuleni katika baadhi ya mataifa ya Ulaya na Marekani, kutokana na madhara ya kiafya yanayosababishwa na kinywaji hicho.

Taarifa zilizotolewa na Shirika la Habari la The Press Television Technology Advertising and Branding (Adweek) zinazonukuu taarifa ya kampuni moja kubwa duniani inayozalisha kinywaji aina ya soda, imeamua kupambana na unene (obesity), unaosababishwa na unywaji wa soda kwa kuondoa matangazo ya vinywaji vyake kwenye vyombo vya habari.

Kampuni hiyo kupitia taarifa yake hiyo iliyotolewa katika moja ya sherehe zake, ilieleza kuwa lengo la kuondoa matangazo hayo ni kuwanusuru watoto wadogo na matumizi ya vinywaji aina ya soda vilivyobainika kuwa na madhara katika mwili wa binadamu.

Nchini Marekani, tayari imekwishapitishwa sheria inayokataza watoto walio na umri wa chini ya miaka 12, kunywa kinywaji aina ya soda.

Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, alieleza kuwa mipango ya mbeleni ya kampuni yake ni kutengeneza kinywaji hicho kikiwa na kiwango kidogo cha Kalori na kubuni kinywaji cha aina hiyo ambacho kitakuwa hakina Kalori.

Alisema mipango hiyo itatekelezwa duniani kote ambako kinywaji cha aina ya soda kinatengenezwa na nchini Marekani tayari imekwishaanza kutekelezwa.

Aidha, Kampuni hiyo imeahidi kuweka wazi virutubisho vyote vinavyotumika kutengeneza bidhaa zake na kuahidi kutoa misaada ya hali na mali kwa nchi zote 200 duniani ambako kinywaji cha soda kinauzwa.

Mbali na Marekani, kinywaji cha aina ya Soda kimekwishapigwa marufuku shuleni katika nchi za Uingereza, Ufaransa na katika majimbo ya Los Angeles, Philadelphia na Miami nchini Marekani na kwa watu wazima matumizi yake yanaelekezwa kuwa ya kiwango kidogo sana.

Vyombo vya habari vya nchini New Zealand, mwezi Machi mwaka huu viliripoti kuwa mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Natasha Harris (31), alifariki kutokana na unywaji wa soda nyingi.

Shirika la habari la AFP la Ufaransa, liliripoti tukio hilo kwa kueleza kuwa Natasha alikuwa akinywa soda nyingi kila siku, jambo ambalo liligeuka kuwa sehemu ya maisha yake kwa kipindi cha miaka mingi.

Kwamba familia ilikuwa ikimuita teja wa soda, baada ya meno yake kuoza kwa sababu ya kunywa soda, alijifungua mtoto ambaye hakuwa na fizi jambo ambalo liligundulika baadaye kuwa lilisababishwa na matumizi makubwa ya kinywaji hicho.

“Tumegundua kwamba, kwa kuzingatia ushahidi uliopo, kama sio unywaji wa soda uliopitiliza, Natasha Harris asingekufa katika muda ule na katika hali alivyokufa

“Ripoti ya Daktari aliyechunguza maiti yake (Pathologia), iligundua kwamba ini lake lilipanuka sana, likawa na mrundiko mkubwa wa mafuta kutokana na kula sukari kwa wingi. Kuwepo kwa madini aina ya ‘potasiam’ kwa kiwango kidogo sana kwenye damu yake, pia kulitokana na unywaji wa soda.” Taarifa ya kitabibu katika Hospitali aliyofia nchini New Zealand ilieleza.



Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kisayansi zilizo kwenye mitandao ya wanasayansi waliobobea duniani, unywaji wa soda humpumbaza mtumiaji na kumsahaulisha kula vyakula vyenye madini muhimu mwilini.

Moja ya andishi linalotahadharisha utumiaji wa kinywaji cha soda na kukitaja kuwa cha hatari kwa matumuzi ya binadamu, ni Jack Winkler, Profesa wa sera za lishe katika Chuo Kikuu cha Metropolitan nchini London, linaloeleza kuwa Soda ni bidhaa ya kishetani inayoua binadamu taratibu baada ya kinywaji hicho kumzalishia magonjwa mengi mwilini yanayomfanya kuwa tegemezi wa dawa.

Wakati msomi huyo akieleza hayo katika utafiti wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Dk. Raymond Wigenge, amelieleza gazeti hili soda siyo kinywaji hatari kwa matumizi ya binadamu kwa sababu kinatumiwa na mamilioni ya watu duniani kote.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano ofisini kwake wiki iliyopita baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu madhara yanayosababishwa na kinywaji aina ya soda katika mwili wa binadamu, Dk. Wigenge alisema pamoja na changamoto zilizopo katika kinywaji hicho, taasisi yake haipingi uwepo wa kinywaji hicho sokoni.

“Soda haina shida kwa binadamu na hata mkiendelea kuandika suala hili, sisi tutaendelea kuueleza umma kwamba waendelee kupata kinywaji, hivyo kama ambavyo tumekuwa tukifanya,” alisema.

Alipoulizwa kama anakubaliana na tafiti za wanasayansi bingwa wa magonjwa ya binadamu walioeleza katika tafiti zao kuwa unywaji wa soda una madhara katika mwili wa binadamu, alisema hizo ni changamoto za kawaida, kwa sababu madhara yaliyomo kwenye soda hayamuathiri mtu mara moja bali huchukua muda mrefu.

Wakati Dk. Wigenge akieleza msimamo wake kuhusu kinywaji aina ya soda, nchini Mexico, taasisi ya El Poder del Consumidor inayojihusisha na kutetea walaji, inashinikiza Serikali ya nchi hiyo kuzilazimisha kampuni za soda kuorodhesha madini na chembechembe zote za kemikali zinazotumika kutengeneza kinywaji hicho.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Alejandro Calvillo, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza kuwa unywaji wa soda ni hatari na hilo limethibitishwa na wataalamu wa afya duniani kuwa soda ni sumu mbaya, inauwa taratibu.

Tafiti mbalimbali za wanasayansi zinaeleza kuwa soda ina asidi aina ya ‘phosphoric’ yenye uwezo wa kuvuruga madini ya ‘calcium’ yaliyoko mwilini na kusababisha mifupa na meno kudhoofika.

Aidha, asidi aina ya ‘phosphoric’ huvuruga asidi aina ya ‘hydrochloric’ iliyo tumboni mwa binadamu na hivyo kuharibu mfumo wa kusaga chakula.

Viwanda vya soda ndio watumiaji wakubwa wa sukari na wanasayansi wanasema sukari hupandisha kiwango cha ‘insulin’ ambayo husababisha kasi ya mzunguko wa damu, ugonjwa wa moyo, kupanda kwa ‘Cholesterol, kisukari, kuzeeka mapema, ongezeko la uzito na maradhi mengine.

Aidha inadaiwa kuwa viwanda vya soda pia hutumia dawa ya kulevya aina ya kafeini. Wataalamu wanasema vinywaji vyenye kafeini, husababisha kupanda kwa mapigo ya moyo, kasi ya mzunguko wa damu na matatizo ya kizazi.

No comments:

Post a Comment