Wednesday, May 15, 2013

KINANA AMTAKA MSIGWA AMUOMBE RADHI HADHARANI, VINGINEVYO WATAMALIZANA MAHAKAMANI...


Katibu Mkuu wa CCM ndugu Abdulrahman Omar Kinana, kupitia kwa wanasheria wa LAW OFFICES OF ERIC S. NG'MARYO wa Moshi amemuandikia Mbunge wa Iringa Ndugu Peter Msigwa agizo la kumtaka amuombe radhi kwa matamshi ambayo kinana anadai ni ya uongo kwamba,


 HII NI SEHEMU  YA  BARUA  HIYO: 
"Nakuandikia kwa maagizo niliyopewa na mteja wangu, Ndugu Abdulrahman Kinana, kufuatia matamshi yako ya uwongo ambayo yamemkashifu, kumfedhehesha na kumshushia hadhi, Matamshi hayo uliyoyatoa mchana wa tarehe 21 April, 2013 katika mkutano wa hadhara wa kisiasa uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza. 


Mkutano huo ulihudhuriwa na watu wengi. Pamoja na watu hao walikuwepo pia waandishi wa habari, wakiwepo wanahabari wa magazeti, radio televisioni. Habari zenye Maneno yako ya Kashfa zimeenea nchi nzima na duniani kote kwa njia ya habari elektoniki, ikiwepo mitandao ya kijamii. 


Habari hizo zinaendelea kusomwa hadi sasa, na zitabaki kuwa kumbukumbu ya kudumu katika intaneti na kwenye hifadhi nyingine za habari"

  "Katika Mkutano huo, ulisikika ukisema maneno mengi ya Kashfa kwa mteja wangu, yakiwemo haya yafuatayo: Kinana (na naomba waandishi w habari mnisikie na nyie usalama wa Taifa mkapeleke habari) hana sifa za kupita barabarani na kuwaambia watanzania waiamini ccm. 

Kinana mikono yake si misafi hata kwenye NASACO, Shirika la Meli Tanzania, kuna harufu ya ufisadi ndani yake, ajibu hapa... Kinana Meli zake ndio zinahusika kubeba mapembe nchi hii, hajajibu hoja hizo! kwa siku katika nchi hii tembo sitini na saba wanauwawa...

Hao ndio wanaokifadhili Chama cha Mapinduzi wakina Kinana halafu wanakuja eti kuwashawishi watanzania muwasikilize na kwamba Chama cha Mapinduzi eti ni kizuri. 

Halafu leo tukikaa ndani ya Bunge tunapojaribu kuwatetea wananchi tumeacha majimbo yetu, Haya mambo ninayaongea ni hatari kwa sababu haya yote ni majangiri ni organized crime ni mtandao wa kimataifa uko duniani kote. unaweza ukatuua lakini wabunge tumesimama tunawatetea.."

Katika  barua  hiyo, mwanasheria huyo  amemtaka Msigwa amuombe msamaha yaishe au la atamvuruta mahakamani, tena kwa vitisho .Nainukuu para  ya mwisho :

"Nakuangaliza na kukutahadharisha kwamba iwapo hutatimiza matakwa ya Mteja wangu kama yalivyoainishwa kwenye barua hii, basi kesi itakayokuja dhidi yako itakuwa na madai makubwa na mengi kuliko yale yaliyotajwa humu, na unaweza kubebeshwa mzigo wa uharibifu, hasara na madhara uliyomsababishia Mteja wangu, pamoja na gharama za kesi nzima, ambazo zote zinaweza kufikia mamilioni ya Shilingi za Kitanzania"

Kuna para  kumi na mbili za barua  hiyo  ambazo zinapatikana ukurasa wa 25 wa gazeti la mwananchi.
 JF

No comments:

Post a Comment